
Huu ndo ukweli kamili kuhusu vifo vya watu sita waliokunywa gongo
Kigogo Sambusa Luhanga Darajani, ambapo wengine wamelazwa wakiwa hoi
katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam umebainika.
Gazeti hili limegundua kuwa gongo waliyokunywa ilikuwa ina mchanganyiko
wa kemikali mbalimbali na dawa za viwandani na tayari sampuli yake
imepelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali kwa uchunguzi zaidi.
Mteja mmoja ambaye kwa kipindi cha nyuma alikuwa ‘mnywaji mzuri’ wa
gongo katika eneo hilo ambaye hakutaka atajwe gazetini alichambua jinsi
pombe hiyo inavyotengenezwa.
Alisema kuwa kuna kemikali zinozotumika kutengezea konyagi ambapo
watengenezaji wanazipata katika kiwanda kimoja (jina tunahifadhi) na
wanachanganya na dawa nyingine.
Alibainisha kuwa kemikali moja hujazwa kwenye chupa ya ujazo wa lita
moja na kuchanganywa na maji kiasi cha lita kumi kisha hutiwa spiriti
pamoja na dawa ya madoa iitwayo ‘jick’ na mchanganyiko huo huzalisha
kitu kinachoitwa gongo na kuanza kusambaziwa wateja.
Chanzo hicho kilisema kuwa njia hiyo ndiyo aliyokuwa akiitumia Hekima
Bakari kwa muda mrefu, mama anayedaiwa kuwauzia gongo watu waliofariki
na kulazwa Hospitali ya Amana.
Kiliendelelea kufafanua kuwa mama huyo ametengeneza mtandao na alikuwa
akisambaza kinywaji hicho Gongo la Mboto, Kipunguni, Chanika, Kitunda,
Kimara Bucha na Kigamboni.
Gongo hiyo ilianza kuua Jumatatu ya wiki iliyopita ambapo ilimuua Juma
Abdallah baada ya kunywa kinywaji hicho na wanywaji wengine wakawa
wanajificha kwa kuwa walikuwa wakiogopa kukamatwa na polisi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa katika eneo hilo la
Kigogo Mbuyuni, Mohammed Mnunga aliwataka wote waliokunywa gongo hiyo
kujitokeza na kwenda kupimwa afya zao kwa usalama wao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Charles Kenyela
amepiga marufuku mtu yeyote kujihusisha na kupika, kuuza au kunywa pombe
haramu ya gongo na akasema tayari watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na
sakata hilo.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa kuwa ni Ramadhan Selestin
(30), Salehe Omary (17), Shukuru Marungu (20), Charles Ibrahim (20),
Fadhili Juma (20) wote ni wakazi wa Kigogo na Abdallah Mnazi (30) mkazi
wa Tabata.
Aliwataja pia waliofariki katika nyakati tofauti kuanzia Julai 7 hadi
12, mwaka huu, katika maeneo ya Kigogo Mbuyuni kuwa ni Juma Abdallah
(60), Mathew Roman (35), Khalid Hamis (31), Mohamed Said (25) na Antipal
Raphel (60) wote wa Kigogo Mbuyuni na Hekima Bakari, ambaye ni muuzaji
wa gongo hiyo.